Pages

CHADEMA HOI MBEYA MJINI, CCM YAZOA 365 KWA MPIGO

Aug 6, 2013


MBEYA, Tanzania
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeisambaratisha ngome ya CHADEMA mjini hapa baada ya wanachama wake 365 wakiongozwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana la chama hicho (BAVICHA), Frank Fumpa.

Wanachama hao walipokewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wazazi Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM , Abdallah Bulembo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Nzovwe Sokoni mjini hapa.

Wengine waliohamia CCM na kurejesha kadi zao kwa Bulembo wakati wa mkutano huo ni wapiga debe maarufu wa chama hicho mjini hapa, Alex Mwaisango na Ambundwile Mwantondo.

Wanachama hao wa CHADEMA waliohamia CCM wakati wa mkutano huo na kupokewa na Bulembo ni miongoni mwa wanachama 375 kutoka vyama vya upinzani wakiwemo wanne kutoka CUF na sita kutoka TLP.

Katika mkutano huo pia Bulembo alikabidhi kadi kwa wanachama wapya wa CCM 279 wakiwemo vijana 15 waendesha pikipiki (Bodaboda), Umoja wa Wazazi Tanzania 15 na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wanachama 15.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake sababu za kuodoka CHADEMA na kuhamia CCM, Fumpa alisema baada ya kutafakari kwa kina kwa muda mrefu walipokuwa ndani ya chama hicho wamegundua hakina mpango wa kuwatetea na kuwaletea maendeleo Watanzania zaidi ya kupanikiza chuki na uhasaba kwa wananchi dhidi ya serikali yao.

Fumpa alisema wakiwa ndani ya chama hicho wameshuhudia mengi ikiwemo msimamo wa viongozi wa chama hicho wa kuwatumia wanachama hususan vijana wa chama hicho kuongoza vurugu na kutokana na vurugu hizo katika baadhi ya maeneo zimesababisha vifo vya watu wasio na hatia.

Alisema wameamua kurejea CCM kwa umamuzi wao bila kushawishiwa na yeyote baada ya kubaini wanapoteza muda mure wa kushiriiana na Watanzania wengine kuharakisha maendeleo yao na kuwashauri warejee CCM kwenye matumaini ya kweli ya ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.

"Zipo kauli za baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wanapowaona wenzao wameamua kurudi nyumbani CCM kuwa wamenunuliwa au kuahidiwa vitu fulani, tuwahakikishie wananchi wenzetu kuwa tumeamua kurejea kwa baba na mama kwa hiari yetu bila kushawishiwa nanyi njooni nyumbani tujenge taifa letu", alisema Fumpa.

Akihutubia mkutano huo, Bulembo aliwataka wananchi wa Jimbo la Mbeya mjini kujutia uamuzi wao waliouchukua mwaka 2010 wa kumchaguae Joseph Mbilinyi 'Sugu'wa CHADEMA kuwa Mbunge wao kwa kutorudia kosa hilo katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.

"Ndugu zangu kufanya kosa si kosa kosa ni kurudia kosa, mwaka 2010 mlimchagua Sugu wa CHADEMA kuwa Mbunge wenu, lakini hawasaidii kuleta maendeleo yenu zaidi ya kuipinga serikali ya CCM kuleta maendeleo, hivyo msirudie kosa hilo katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na uchaguzi mkuu mwaka 2015", alisema Bulembo.

Bulembo aliyeko katika ziara ya kukagua, kuhimiza uhai wa Chama na jumuia zake, kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM mkoani hapa alisema kuchagua upinzani ni kuthoofisha jitihada za serikali ya CCM ya kuharakisha maendeleo yao.

Alisema vyama vya upinzani kikiwemo CHADEMA haitakii mema CCM na vimekuwa vikifanya kila liwezekanalo kuhakikisha ilani ya CCM inayolenga kuondoa kero na changamoto zinazowakabili wananchi haitekelezwi, hivyo kuchagua upinzani ni sawa na kusitisha kwa muda maendeleo yao.