Pages

Mfanyakazi wa Barrick mwaathirika wa kemikali afariki

Oct 29, 2012

 Samuel alifariki Oktoba 25  saa 2:00 usiku. 
MFANYAKAZI wa Kampuni ya Africa Barrick Gold aliyekuwa akifanya kazi mgodi ya Bulyanhulu, wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga, Samuel Kamudulu amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu akisumbuliwa na mapafu na uti wa mgongo.
Akizungumza kwa simu kutoka Arusha, kaka wa marehemu, Lekiu Kamdulu  alisema Samuel alifariki ghafla walipokuwa Arusha baada ya kutoka matibabu Dar es Salaam.
“Samuel alifariki Oktoba 25  saa 2:00 usiku. Unajua baada ya kumwandikia ile habari kwenye gazeti la Mwananchi, kampuni ilimchukua na kuanza kumtibu. Kwa hiyo tuliitwa Kahama tukafanyiwa utaratibu na kurudishwa tena Dar es Salaam kwenye matibabu,” alisema Kamudulu na kuongeza:
“Baada ya kutoka kwenye matibabu tulikuja Arusha nyumbani tangu wiki iliyopita hadi alipofariki juzi.”  
Wakati wa uhai wake, Samuel alisema mapafu yake yameathiriwa na kemikali zinazotumika kwenye uchimbaji madini ya dhahabu.
“Mapema mwaka huu nikiwa kazini ndani ya mgodi niliishiwa nguvu ghafla na kuanguka. Nilibebwa bila kujitambua na kupelekwa hospitali ya kazini na kuambiwa kuwa nina ugonjwa wa mapafu (pneumonia),” alisema Samuel wakati wa uhai wake na kuongeza:
“Baada ya hali kuzidi kuwa mbaya nililetwa Hospitali ya Aga Khan ambako nimeambiwa mapafu yangu yameoza kutokana na kemikali zinazotumika mgodini.”
Alipoulizwa kuhusu kifo hicho, Ofisa Habari wa Barrick, Nector Foya alisema hana taarifa za kifo cha mfanyakazi huyo.