Pages

Tuliwakumbusha, CCM Wajihadhari Na ‘Fedha Za Bhangi

Oct 26, 2012

 SIKU zote Waswahili wanasema: “Msemea sikioni siyo majinuni!” Hata hivyo, ni wachache wanaoweza kuzingatia yale wanayoambiwa na daima wanapoyafanyia kazi huwa wanapata matokeo mazuri. 
Suala la rushwa ndani ya Chama cha Mapinduzi limekuwa sugu, wenye fedha wamekuwa wakilangua kura ili kupata uongozi, hata kama hawana sifa stahiki. Lakini pamoja na ‘Wenye hekima wa Babeli’ kutahadharisha madhara ya mchezo huo mchafu, bado wahusika wameziba masikio kwa nta, hawataki kusikia la Muadhini wala Mnadi Swala! 
Matokeo yake CCM limekuwa kokoro kama alivyopata kusema Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Kokoro linalovua samaki na konokono kwa pamoja, na inahitajika busara na hekima kuweza kuchambua samaki na konokono hao ambao ni hatari mno. 
Uongozi ndani ya CCM ni sawa na kutangaza zabuni, ambayo mwenye fedha nyingi ndiye anayeshinda na kupewa uongozi huo. Rushwa imekuwa kansa mbaya ndani ya CCM, fedha zinamwagwa nje nje na viongozi wao wanaangalia na kuchekelea, wanakemea rushwa na tabasamu pana kana kwamba ni kitu cha kawaida tu. Hii ni aibu kwa chama kikongwe na chenye dhamana ya kuongoza Taifa!