Pages

Ndege 8 kubwa za Obama Zatua Dar

Jun 28, 2013

Mmoja ya Madege ya Marekani yaliotua Tanzania.Dar es Salaam, Tanzania.Makachero wa Marekani wameendelea na matayarisho ya mwisho ya ziara ya Rais Barack Obama, na katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere walikuwa na kazi ya kuunganisha helikopta za doria.


Makachero hao walikuwa wakiunganisha helikopta sita zilizosafirishwa vipande vipande kutoka Marekani, ambapo meli mbili za kivita na ndege moja pia zimewasili.


Rais Obama tayari yuko katika ardhi ya Afrika, na  leo anatarajiwa kwenda Afrika Kusini baada ya kumaliza ziara yake ya kwanza Senegal na anatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu.


Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa jana unaonyesha Marekani imeleta helikopta hizo kwa ajili ya ulinzi wa Rais Obama, zikiwamo meli zilizobeba helikopta nyingine mbili na ndege.

Habari zilizopatikana kutoka kwa wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, zinasema kuwa helikopta sita zinaunganishwa katika sehemu ya karakana ya Kikosi cha Anga cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Mtu mmoja amesema helikopta hizo zililetwa kama vipande vipande vilivyosafirishwa kama mzigo kwenye meli za kivita zilizotia nanga jijini Dar es Salaam.


“Nilikaribia kwenye eneo la karakana na nikashangaa kuona jinsi jamaa walivyokuwa ‘bize’ wakiunganisha vyuma mbalimbali na kutengeneza helikopta hizo,” amesema mtu huyo.


Inaaminika kuwa helikopta hizo zitakuwa zinasaidia kusafirisha watu na mizigo kutoka kwenye meli za kivita ambazo zimeegeshwa kwenye Kikosi cha Maji cha JWTZ.

Pia helikopta mbili zinaaminika ziko katika meli ambazo zimeegeshwa huko Kigamboni.


Meli za kivita na ndege ya kijeshi


Katika hatua nyingine, meli mbili za kivita ambazo zimetengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu zimeegeshwa Kigamboni.

“Jamaa wana meli kali kwa kweli, mimi nimekuwa askari wa Kikosi cha Maji kwa muda mrefu na kufanya mazoezi na mataifa kadhaa, lakini sijaona meli kama zile.

“Wamarekani wanatisha sana. Meli zao zina zana muhimu za kivita. Pia wanafuatilia kila kitu kinachoweza kuhatarisha usalama wao. Hawaamini mtu kabisa wala kudharau chochote,” amesema mtoa habari mmoja.

Ndege ya kijeshi

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kuna ndege ya Jeshi la Marekani, lakini imeegeshwa kwenye karakana ya Kikosi cha Anga cha JWTZ.


Ndege hiyo inadaiwa iko nchini tangu mwanzoni mwa wiki hii, ingawa kuna taarifa kuwa zipo ndege nyingine ambazo zimekuwa zikitua na kuruka.


“Ndege nyingi za Wamarekani zinatua nchini kwa kipindi cha wiki mbili sasa, zaidi zinaleta watu, ambao nahisi ni wale wanaohusika na usalama na mizigo.


“Kimsingi kuna mambo mengi yanaendelea hapa uwanja wa ndege. Ila msisahau pia kuna ujio wa marais kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya mkutano wa Smart Partnership ndiyo maana kuna mengi yanaendelea hapa,”  chanzo cha habari kimesema. Chanzo: Mwananchi.co.tz