Makamanda watano wa Chadema wakiingizwa ukumbi wa mahakama ya hakimu mkazi mkoani Tabora kufuatia kesi ya Ugaidi inayowakabili akiwemo kaimu Katibu wa Chama hicho mkoa wa Dar-es-Salaam Bw.Henry Kileo aliyeshika Kitabu mkononi.
Wanachama watano wa chama cha Demokrasia na Maendeleo- CHADEMA wanaokabiliwa na mashitaka ya Ugaidi wamerejeshwa tena rumande pasipo maombi yao kusikilizwa hadi tarehe 22/07/2013 kesi hiyo itakapotajwa tena.
Akitoa uamuzi huo hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya mkoa wa Tabora Issa Magoli amesema kuwa kwa vile mahakama yake haina uwezo kisheria kusikiliza shauri hilo kesi hiyo inahairishwa hadi hapo upande wa utetezi wakiendelea na taratibu za kupeleka hoja zao Mahakama kuu.
Hakimu Magoli kabla ya kuahirisha shauri hilo aliwashauri mawakili wa upande wa utetezi wawasilishe hoja zao mahakama kuu ya Tanzania ndipo watakapoweza kupatiwa ufumbuzi wa kisheria.
Akizungumza nje ya Mahakama,Wakili wa washtakiwa hao,Peter Kibatala,alisema wanafanya utaratibu wa kupeleka shauri lao Mahakama Kuu baada ya kupewa nakala ya uamuzi uliotolewa na mahakama ya hakimu Mkazi Tabora.
Alisema katika maombi yao Mahakama kuu wataomba ipitie shauri hilo na pia kuona kama ni halali kisheria kwa washtakiwa hao kufunguliwa kesi hiyo baada ya awali washtakiwa wanne ukimuondoa Kilewo mashtaka yao kuondolewa na kasha kushtakiwa tena na Kilewo.
Wakili Kibatala mbali ya kusema ana imani na Mahakama lakini alieleza wana Imani zaidi na mahakama Kuu kwa vile alidai ipo huru
Alisisitiza kama mawakili wa washtakiwa wanapambana kuhakikisha haki inatendeka na kuwaomba wana ndugu na jamaa kuwa watulivu na wawategemee.
“Nawaomba ndugu na jamaa wa washtakiwa kuwa watulivu wakituacha mawakili wao tukipambana katika suala hili na tunawatia moyo msikate tama kwani kesi ni suala la mchakato na linaweza kuchukua muda mrefu”Alisema
Kwa upande wake Mke wa mshtakiwa Henry Kilewo,Joyce Kiria,alisema yeye alipoamua kuolewa na Kilewo alijua ni mwanaharakati lakini kwa vile anampenda alikubali kuolewa naye.
Alisema yupo naye katika kipindi hiki na bado anampenda na kuwatia moyo wanawake kuwa bega na waume zao pale wanapokuwa na matatizo.
“Nataka niwaambie kuwa hii sasa ndio wanawake live ni lazima wanawake tuwe wavumilivu katika kupambana na tusibaki kulia lia”Alisema.
Shauri hilo lilivutia umati wa wapenzi wa CHADEMA waliojitokeza kwa wingi huku ulinzi ukiwa mkali ambapo Askari wa kikosi cha kutuliza Ghasia walitanda wakiwa na silaha.
Watuhumiwa hao watano akiwemo kaimu katibu wa Chadema Bw.Henry Kilewo,Evodius Justian,Oscar Kaijage,Seif Kabuta na Rajabu Kihawa wamerejeshwa rumande hadi hapo tarehe 22 Julai mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.|Na KapipiJHabari