CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemtaka Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kueleza kama msimamo alioutoa katika kampeni za Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga ni wa Serikali au wake.Chama hicho kimesema kuwa msimamo alioutoa Magufuli wa kuunga mkono Chama cha ODM ni hatari kwa Tanzania hasa katika uhusiano na nchi hiyo na ni kinyume na mkataba wa kimataifa wa Rome.
Pia kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kueleza kama alimtuma Magufuli katika mkutano huo wa kampeni uliofanyika Desemba 7 mwaka huu, uwanja wa Kasarani na kusema Watanzania wanaunga mkono ODM au la.Msimamo huo wa Chadema ulitolewa jana na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa chama hicho, Ezekieah Wenje.
“Hatujui kama Magufuli alikwenda Kenya kama Serikali au alikuwa amekwenda kama rafiki. Hilo linatupa wasiwasi kwa kuwa hotuba yake ilionekana kama ametumwa na Serikali,” alisema Wenje na kuongeza;
“Alichukua upande katika siasa za Kenya, alimsifia sana Odinga kwamba Tanzania wanampenda wakati kuna mikataba ya kimataifa inayokataza nchi nyingine kuingilia siasa za nchi nyingine kama ilivyoelezwa kwenye Rome Statute.”