UNAWEZA kusema dunia sasa iko ukingoni inasubiri siku ya hukumu kwani matukio yasiyo ya kawaida yamekuwa mengi kila kukicha.
Desemba 8, mwaka huu, mwanafunzi wa darasa la pili, katika Shule ya Msingi Mbata jijini hapa aliyejulikana kwa jina moja la Sharifu amejikuta katika wakati mgumu kiasi cha kuangua kilio baada ya kutelekezewa kichanga.
Kwa mujibu wa mtoto Sharifu mwenyewe, siku ya tukio, saa nne asubuhi alikuwa akitoka shuleni kwenda nyumbani na ndipo alipokutana na kisanga hicho.
Alisema akiwa hajatembea umbali mrefu kutoka shuleni hapo, mwanamke mmoja akiwa na kichanga mgongoni alimwita na kumwomba amsaidie kumbeba kwa muda yeye anarudi nyumbani kuchukua kitu alichosahau.
Denti huyo aliongeza kuwa, alikubali ambapo alikaa chini na kumtwaa mtoto huyo kisha kumpakata akiamini muda si mrefu mama mtu angerejea na kumchukua.
Mwanafunzi huyo akasema muda ulipita mama wa mtoto akiwa hajarudi na mbaya zaidi, mtoto huyo alianza kupaza sauti ya kilio kama inavyokuwa kawaida kwa watoto wachanga.
“Nilipoona mtoto analia sana na mama yake hatokei na mimi nikaanza kulia. Ndipo alipotokea mwanafunzi mwenzangu mmoja na kuniuliza kwa nini nalia? Nikamsimulia yaliyonipata,” alisema Sharifu.
Alisema mwanafunzi huyo alitoa wazo la kumchukua mtoto huyo hadi shuleni ili wakambwage kwa walimu ambao na wao watajua wenyewe pa kumpeleka.
Pale shuleni, walimu waliposimuliwa kisa kizima na Sharifu akichagizwa na mwanafunzi mwenzake huyo, walichukua uamuzi wa kumpeleka mtoto huyo kituo cha polisi ambapo mpaka Jumapili iliyopita mama yake alikuwa hajapatikana.
Mwalimu mmoja wa shule hiyo, Upendo Mwakipunda alikiri kujiri kwa tukio hilo ambapo alisema suala zima kwa sasa liko mikononi mwa polisi