FEDHA ZA MATIBABU ZAPATIKANA,MADAKTARI WAKATAA MSAADA WA SERIKALI.
Geofrey Nyang’oro
MWENYEKITI
wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka amesafirishwa
kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.Kusafirishwa
kwake kunafuatia hatua ya jopo la madaktari waliokuwa wakimhudumia,
kueleza mabadiliko ya hali ya afya yake, yaliyosababisha figo kushindwa
kufanya kazi, hali iliyolazimu pamoja na matibabu mengine, kwenda
kusafishwa damu.
Ingawa
madaktari hao wamekataa kuweka wazi nchi anayopelekwa, kuna taarifa
kwamba huenda amesafirishwa kwenda nchini Afrika Kusini.
Katika
Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) jana makundi mbalimbali ya watu
yalifurika wakiwamo wanaharakati na ndugu wa Dk Ulimboka, waliofika kwa
lengo la kumsindikiza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Watu hao waliofika hospitalini hapo kuanzia asubuhi, waliendelea kubaki eneo hilo hadi saa 6:45 mchana msafara ulipoanza.
Dk
Ulimboka alisafirishwa kwa gari la kubebea wagonjwa la kampuni ya AAR.
Alipofika uwanjani, alisafirishwa kwa ndege ya kukodi ya Shirika la
Ndege la Afrika Kusini, akisindikizwa na watu watatu.
Usiri safari ya Dk Ulimboka
Mapema
jana asubuhi, taarifa za kusafirishwa kwake zilizagaa, lakini hapakuwa
na mtu wa kuthibitisha safari hiyo na namna atakavyosafiri.
Katika
safari hiyo, Dk Ulimboka amesindikizwa na Dk Pascal Lugajo, kaka yake,
Dk Hobakile Ulimboka na mke wake, Dk Judith Mzovela.
Madaktari watoa tamko
Baada
ya Ulimboka kusafirishwa, madaktari walilaani kitendo cha kutekwa na
kupigwa mwenzao na kuitaka Serikali itoe tamko juu ya usalama wao.
Katibu
wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Edwan Chitage aliwaambia waandishi
wa habari kuwa tukio hilo na vitisho vya kufukuzwa kazi wanataaluma hao
kunakofanywa na Serikali, kumezua hofu kwa madaktari wote nchini.
“Tunaamini
Serikali inawajibika kwa watu wake, kwa hali ilivyo sasa madaktari wapo
kwenye hofu kubwa, tunataka itoe tamko juu ya usalama wa madaktari,”
alisema Dk Chitage.
Akizungumzia
hali ya Dk Ulimboka, alisema imekuwa ikibadilika mara kwa mara hali
ambayo imesababisha kumpeleka nje ya nchi kwa matibabu zaidi .
Chitage
alisema kama Serikali ingekuwa na nia ya kuboresha huduma hospitalini
hapo ingeweza kununua mashine ya CT Scan ambayo alisema bei yake ni sawa
na Toyota ‘Shangingi’ moja.
Kwa
upande wao wanaharakati wa haki za binadamu, jana walifika Uwanja wa
Ndege wakiwa na mabango yenye ujumbe tofauti wakilaani kitendo
alichofanyiwa Dk Ulimboka.
Dk
Chitega alisema hadi kufikia jana, walikuwa wamepata fedha zilizokuwa
zikihitajika kwa ajili ya matibabu yake. Juzi madaktari hao walisema
wanahitaji Dola za Marekani 40,000 (Sh63.2 milioni) ili kumtibu mwenzao
nje ya nchi.
Serikali na tiba ya Ulimboka
Wakati mgomo wa madaktari ukiingia siku ya nane leo, Serikali imesema ilikuwa tayari kugharimia matibabu ya Dk Ulimboka.
Msemaji
wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja jana alisema
Serikali ilikuwa tayari kugharimia matibabu ya daktari huyo.
Mwamaja aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa ni haki ya mgonjwa anayepewa rufani ya kutibiwa nje, kugharimiwa na Serikali, lakini
msaada huo wa Serikali ulikataliwa na madaktari hao na kuitaka ikae mbali na matibabu ya kiongozi wao.
“Sisi
tulishaanza maandalizi ya kugharimia matibabu yake, lakini madaktari
wenyewe walikataa msaada wa Serikali,” alisema Mwamwaja.
Hali yazidi kuwa tete
Kutokana
na mgomo huo, uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi,
umewatimua zaidi ya madaktari 80 walioko kwenye mafunzo kwa vitendo.
Hadi
kufikia juzi, madaktari 146 walikuwa wamefukuzwa kutokana na mgomo huo
katika hospitali za Bugando na Sekou Toure mkoani Mwanza na Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Mbeya na ile ya Mkoa wa Dodoma.
Mbeya
Habari
kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mbeya zinadai kwamba, baada ya uongozi wa
hospitali hiyo kulazimika kuomba madaktari wengine kutoka hospitali za
jijini Mbeya ili kuongeza nguvu, madaktari hao nao wameonekana
kutoridhishwa na ombi hilo.
Habari
hizo zinasema kwamba, licha ya madaktari hao kupatikana na kwenda
hospitalini hapo, walisikika wakilalamika kwamba wao hawapo tayari
kufanya kazi sehemu yenye mgogoro na kwamba wao hawawezi kufanywa kama
chambo kwa kuhofia usalama wao.
Akizungumza
kwa njia ya simu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk Eliuter Samky
alikiri kuzidiwa na kusuasua kwa utoaji huduma kwa wagonjwa ambapo
alisema kuwa hadi sasa huduma zinazotolewa ni zile za dharura pekee na
zile za kawaida wagonjwa wanaambiwa waende Hospitali ya Mkoa.
Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Dk Seif Mhina, alisema kwa sasa
hali inaendelea vizuri kutokana na kujipanga vyema kukabiliana nayo,
licha ya kuwa bado kuna tatizo la upungufu wa vitanda hivyo kusababisha
wagonjwa kulala chini.
Tanga
Baadhi
ya wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, wameitaka
Serikali kukaa pamoja na madaktari ili kumaliza tatizo hilo.
Wamesema
hali iliyofikia sasa ni mbaya hivyo ni busara pande hizo mbili kukaa
meza moja kutatua mgogoro huo bila kujali nani kati yao amesababisha.
Sakina
Abdallah ambaye amelazwa katika wodi ya wazazi ya Gallanis, alisema
amesikitishwa na baadhi ya wanasiasa wanaoshabikia kutekwa Dk Ulimboka.
“Binafsi
hali inayoendelea ya mgomo wa madaktari inanihuzunisha sana kwani
tunaoumia ni sisi wananchi tunaotibiwa katika hospitali hizi,” alisema
Sakina.
Godfrey
Jambia ambaye ni majeruhi aliyelazwa katika hospitali hiyo, alisema
Serikali inatakiwa kutatua madai ya madaktari hao ili kuwanusuru raia
wasio na hatia.
NCCR yaivaa Serikali
Chama cha NCCR-Mageuzi kimesema Serikali ina maswali ya kujibu kutokana na kushindwa kutatua mgomo wa madaktari nchi nzima.
Chama
hicho kimesema Serikali haitakiwi kutumia nguvu ya dola kumaliza mgomo
na kuitaka ifute kesi iliyofunguliwa mahakamani ili kukaa meza ya
majadiliano na madaktari hao kwa kuwa raia wasio na hatia, wanapoteza
maisha kwa kukosa matibabu.
Akizungumza
wakati akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu (Nec) ya chama hicho Dar es
Salaam jana, Mwenyekiti wa chama, James Mbatia, alisema hata kama suala
hilo limefika mahakamani, bado linazungumzika kwa kuwa afya za
Watanzania zinawahusu wote.
“Hivi
Serikali inashindwa kuliondoa jambo hilo mahakamani na kukaa meza moja
na madaktari kumaliza tatizo hili..., katika hili lazima tuseme, yaani
watu wanakufa tukae kimya, haiwezekani hata kidogo,” alisema Mbatia na
kuongeza:
“Ubabe
hauwezi kuingizwa katika uhai wa Watanzania, kama majadiliano ya awali
hayakufanikiwa basi wawekwe watu makini watakaosimamia majadiliano haya,
hata wabunge wanaweza kusimamia suala hili, mgomo huu hauna itikadi za
vyama unawahusu wananchi wote.”
Habari Hii imeandaliwa na Fidelis Butahe, Claud Mshana, Dar, Burhani Yakub,Tanga na Godfrey Kahango, Mbeya