Pages

Wabunge Wote Vijana Kupigishwa Kwata JKT

Jul 17, 2012

  Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha akiwasilisha bungeni hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/13, mjini Dodoma jana.

WABUNGE vijana walioko katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watapaswa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa Mujibu wa Sheria kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2012/13.
Waziri wa Ulinzi na JKT, Shamsi Vuai Nahodha alisema hayo alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya wizara yake bungeni jana. Alisema wabunge vijana watakuwa sehemu ya kundi la kwanza la vijana 5,000 katika mafunzo yatakayoanza Machi, mwakani.

Alisema wizara hiyo imelifanyia kazi ombi la kuandaa mafunzo ya JKT kwa wabunge vijana kama ilivyoombwa mwaka jana na kwamba wabunge hao wameandaliwa mafunzo hayo ya wiki tatu.
“Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu imelifanyia kazi ombi hilo na kuandaa utaratibu wa mafunzo maalumu ya wiki tatu kwa waheshimiwa wabunge vijana,” alisema Nahodha na kuongeza:

“Kwa hiyo wabunge vijana wataungana na kundi la kwanza la vijana 5,000 niliowaeleza hapo juu… naomba waheshimiwa wabunge mjiorodheshe kwa maandalizi ya mafunzo haya.”
Waziri Nahodha alisema ni imani yake kuwa, pamoja na wabunge kunufaika na mafunzo hayo, watahamasisha urejeshwaji wa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria na kutoa taswira nzuri ya mafunzo hayo kwa jamii.

Alisema JKT tayari imefanya maandalizi ya kutosha na kwamba kambi tano zenye uwezo wa kuchukua vijana 20,000 kwa wakati mmoja zimeshaandaliwa kwa ajili hiyo.
Alizitaja kambi hizo kuwa ni Bulombora na Kanembwa za mkoani Kigoma, Mlale ya Ruvuma, Msange mkoani Tabora na Oljoro hukoArusha.

Hata hivyo, alisema gharama ya kuendesha mafunzo hayo ni kubwa hivyo JKT haitaweza kuchukua vijana wote na ndiyo maana imeamua kuanza na hao 5,000.
“Vijana hao ni miongoni mwa vijana 41,348 ambao watahitimu mafunzo ya kidato cha sita katika mwaka 2013,” alisema Nahodha.

Kuhusu utaratibu wa kujiunga na kambi hizo, Nahodha alisema uandikishaji wa vijana shuleni utafanyika kati ya Desemba mwaka huu na Januari 2013 na kwamba kambi zitawapokea kati ya Machi 7 na 16, mwakani.Alisema mafunzo hayo ya miezi sita yataanza Machi 17 mwakani na kuendelea hadi Agosti 16.