Maiti ya Kijana Rashid Juma aliyepigwa risasi na askari polisi ikiwa imelazwa katika chumba cha kuifadhia katika hospitali ya Wilaya ya Bukombe.
BUKOMBE
Mtu mmoja anayeitwa Rashid Juma (23) ameuawa kwa kupigwa risasi na askari polisi katika kitongoji cha Kilimahewa kilichoko mjini Ushirombo wilaya ya Bukombe mkoani Geita leo(Nov 24) Asubuhi.
Marehemu Juma amedaiwa kupigwa risasi na askari polisi wakati walipokuwa wanakamata mtu, anayesadikiwa kuwa ni jambazi, aliyekuwa amejificha kwenye nyumba moja katika kitongoji hicho.
Mwandishi wetu ameripoti kuwa, baada ya askari kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo, wananchi wenye hasira walilivamia gari la polisi kwa nia ya kumuua, hali iliyosababisha askari waanze kupiga risasi za juu ili kuwatawanya.
Imeelezwa kuwa katika tafrani hiyo, marehemu aliokotwa na wananchi akiwa amejeruhiwa kiunoni kwa kitu kinachohisiwa kuwa ni risasi ya moto, kabla ya kubebwa na wananchi hao kwa maandamano hadi kituo cha polisi.
Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dk. Archard Rwezahura ameleza, marehemu Juma amefariki kabla yakufikishwa hospitalini hapo na kwamba mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita Lenard Paul amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba hatua za kisheria zinafuatiliwa.
MATUKIO KATIKA PICHA
Askari polisi akijitahidi kuwatawanya wananchi waliokuwa na hasira
Moshi wa bomu la machozi ambalo lililirushwa na askari polisi wa kituo hicho kwa ajili ya kuwatawanya wananchi ambao walikuwa na lengo la kuvamia kituo.
Msafara wa Mbunge, wa Bukombe, Profesa Kulikoyela Kahigi Pamoja na Diwani na baadhi ya askari na wananchi wakiwa wanaongozana kwenda katika hospitali ya Wilaya ya Bukombe kwa ajili ya kuangalia mwili wa marehemu Rashid Juma aliyepigwa risasi na polisi na kufa hapo
Mbunge wa Bukombe Profesa, Kulikoyela Kahigi Chadema (Kulia) akipokea maelezo kutoka kwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Bukombe Dk. Archard Rwezahura, (aliyevaa shati la kitenge) jinsi alivyopokea maiti ya kijana huyo ambaye alipigwa risasi na Polisi na kufikishwa hospitali hapo akiwa amefariki.
SOURCE SHOMARI BINDA BLOG