Sikia nikuambie rafiki yangu, huna haja ya kumuacha mumeo/mkeo kutokana na usaliti, nasema hivyo nikiwa nina imani kwamba, kwa mada hii, utapata maarifa mapya. Hii mada imekuwa na maoni mengi sana.
Wapo ambao wamekuwa mifano ya moja kwa moja ya kile nilichotaka kukizungumza leo, kwa maneno mengine, kuna waliochangia yale ambayo nilipanga kuandika leo. Kutokana na hilo, nitakwenda moja kwa moja katika maoni ya mmoja wao kutokana na nafasi kuwa finyu. Twende tukaone...
Anasema: Habari za kazi? Mimi ni mama, nimeishi kwenye ndoa kwa miaka 22 sasa, kweli ndoa ina kazi, lakini inabidi ukiwa kama mama ujipange, uweze kumwangalia mume na pia watoto. Mume ana nafasi yake na watoto nao wana nafasi yao ila wamama tunapenda mambo ya kibishoo na kuiga, tunasahau majukumu yetu. Mimi nilikuwa sijui wajibu wangu, nimesoma magazeti yenu sana, yamenifunza mambo mengi, nimerekebisha kila kitu ambacho kilikuwa kinaleta ugomvi. Mume wangu ananiheshimu na mimi pia namheshimu, mwanaume bwana ukimlea yeye na watoto wake vizuri sidhani kama ataacha kukupenda. Mfano, unatakiwa uamke mapema, umwandalie kifungua kinywa kabla hata hajaamka.
Umwamshe na kumpelekea huko huko chumbani, kahawa, maziwa au juisi. Nafanya hayo yote mimi mwenyewe nikiwa tayari nimeshaoga, ni msafi namvutia mume wangu. Mara nyingine huwa anashawishika kunihitaji, nami sikatai, nafanya hivyo ili asipate visingizio vya kutoka nje.
Naishi naye kama rafiki, wakati mwingine tunazungumza mambo mbalimbali, ya binafsi na ya kifamilia. Tunaishi vizuri, anawahi kurudi nyumbani maana anajua kuna mke anayemjali. Mwanaume unatakiwa kumfanya kama mtoto.
Mume wangu ni mfanyabiashara na mimi ni mfanyakazi, kwahiyo mara nyingi asubuhi yeye huwa anabaki akiwa bado amelala, lakini nahakikisha simwachi peke yake kiakili, kila wakati namchokoza kwa meseji au simu.
Wanawake tubadilike, dada yangu (aliyechangia wiki iliyopita) acha presha, badilisha mfumo wa maisha utaona. Hata kama utaachana naye, utaenda kwa nani, wanaume wanafanana mama! Utaolewa na wangapi? Achana na mambo ya mahausigeli, fua nguo za mumeo, nyoosha, mtengee maji bafuni, mpikie na umfanye ajisikie yupo na mwanamke makini. Watoto wasizuie nafasi ya mume, watoto wawe wa kawaida lakini mume awe mpya kila siku.
Nina watoto watatu sasa na tunaishi vizuri tu. Ukiwa mkarimu kwa mumeo, watoto unawapa malezi bora, mumeo atakusaliti kwa lipi?
UMEJIFUNZA NINI?
Nadhani kuna jambo mmejifunza kupitia maoni ya mama huyo ambaye hapa nimeficha jina lake. Usaliti ingawa wakati mwingine ni hulka ya mtu, lakini ukiweza kumpa kila kitu mpenzi wako unakuwa umemloga moja kwa moja.
Hana ujanja, ataenda wapi wakati anapata kila kitu kwako? Jifunze kutokea hapo na uchukue hatua. Je, wewe una maoni gani?