Pages

Malawi kubatilisha sheria ya mapenzi

May 18, 2012
Rais Joyce Banda


Rais wa Malawi,Joyce Banda amesema kuwa anataka nchi hiyo ibatilishe sheria inayoharamisha ndoa za jinsia moja na kuifanya nchi ya kwanza ya kiafrika kufanya hivyo tangu mwaka 1994.
Wananume wawili raia wa nchi hiyo walihukumiwa kifungo cha miaka 14 gerezani mwaka 2010 baada ya kutangaza kuwa wanataka kuoana.
Baadhi ya viongozi wa nchi za magharibi, hivi karibuni wametishia kusitisha msaada kwa nchi za kiafrika ambazo hazitatambua haki za mashoga.
Rais Banda alichukua hatamu za uongozi mwezi jana kutoka kwa mtangulizi wake, Bingu wa Mutharika, aliyeaga dunia kutokana na mshtuko wa moyo.
Hadi sasa rais huyo amegeuza baadhi ya sera zake ikiwemo kushusha thamani ya sarafau ya nchi kwa lengo la kuanza kupata msaada .
Wafadhili wengi walisitisha msaada chini ya utawala wa Mutharika, wakimtuhumu kwa uongozi duni pamoja na ukandamizaji.
Katika hotuba yake ya kwanza kwa bunge la anchi Banda alisema kuwa baadhi ya sheria zilizopitishwa na bunge, zitafutiliwa mbali kama hatua ya dharura ikiwemo sheria zinazopinga vitendo visivyo vya kawaida.
Mwandishi wa BBC Raphael Tenthani mjini Blantyre, anasema kuwa rais anaungwa mkono na wabunge wengi, na kwa hivyo ataweza kuwashawishi wabunge kubatilisha sheria hiyo.